KLABU ya Simba imekubali mwaliko wa kwenda kucheza mechi ya kirafiki na Timu ya Polisi Dodoma ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli za kuhamia Mkoani Dodoma.
Mwaliko huo umeletwa na Chama Cha Soka Mkoa wa Dodoma kupitia kwa Mwenyekiti wake, Mulamu Nghambi ambaye amesema kuwa wao kwa pamoja wanaunga mkono juhudi za Rais za kuhamishia makao makuu ya nchi mkoani kwao kwani zitaleta maendeleo makubwa.
Nghambi amesema, walituma maombi yao kwa uongozi wa klabu ya Simba wa Kuonesha nia ya kushirikiana katika harakati hizo kwani mkoa wa Dodoma una mashabiki wengi wa timu ya Simba na mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Septemba 03 kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) Mulamu Nghambi akizungumza na waandishi wa habari akielezea kuhusiana na kuunga mkono juhudi za Mheshima Raisi John Magufuli za kuhamishia makao makuu mkoa wa Dodoma Kulia ni Mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba Haji Manara.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara amesema kuwa wamefurahi kupata mwaliko huo na kwa kuwa hakuna ratiba ya ligi wikiend hii nawaahidi mashabiki wa Simba mkoani Dodoma kusubiri ujio wetu kwa shangwe zote.
“Katika kuhakikisha tunaunga mkono hoja za Rais John Pombe Magufuli za kuhamishia makao makuu ya nchi Mkoani Dodoma na Chama cha Mpira wa Miguu mkoani humo kutupatia mwaliko tumeupokea kwa mikono miwili na tunawataka wanachama na mashabiki wa timu ya Simba kuja kushuhudia mchezo wetu na Polisi Dodoma siku ya Jumamosi Septemba tatu mwaka huu,”amesema Manara.
Kikosi cha Simba kitaondoka Alhamisi wakiwa na wachezaji wao wote waliosalia baada ya wengine kuwepo kwenye majukumu ya timu zao za Taifa.
Post a Comment